Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linamsaka dereva
aliyempa rushwa ya Sh. 5,000 askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani
ambaye amefukuzwa kazi, kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.
Katikati
ya wiki, video fupi iliyokuwa ikionyesha askari huyo akipewa rushwa na
dereva wa gari ndogo ilisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na
kusababisha Polisi kumchukulia hatua trafiki huyo.
Kamanda
wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliwaeleza
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam "video ile" iliwashutua na
walichukua hatua mara moja za kumfukuza kazi na sasa ni raia wa
kawaida.
Juzi
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi
Jumanne Murilo, alisema askari huyo alifukuzwa tangu Jumanne.
Kamanda
Murilo alisema askari huyo hadi anafukuzwa kazi ndani ya Jeshi la
Polisi alikuwa amefanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.
"Tukio
hili lilifanyika eneo la Mwenge na baada ya kulibaini tulianza
uchunguzi wetu ambao juzi (Jumanne) ulikamilika na kubaini tukio hilo
lilikuwa la kweli (kwamba) amepokea rushwa. Hivyo tumemuondoa kazini,"
alisema juzi Kamanda Murilo.
Kamanda
Murilo ambaye hakumtaja jina askari huyo aliwakumbusha trafiki
kuzingatia maadili ya kazi na taratibu za kijeshi zilizowekwa.
Akirejea taarifa hizo, Mambosasa alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea .
"Kwa sasa upelelezi unaendelea ili kumfikisha mahakamani mtuhumiwa ambaye kwa sasa si askari tena," alisema Kamanda Mambosasa.
"Lakini
kama ambavyo sheria za rushwa zinavyoelekeza ni lazima tumpate na
aliyehusika kutoa rushwa ili kupata ushahidi wa kesi hiyo," alisema
Mambosasa.
Alieleza
zaidi kuwa ingawa wanamsaka mtuhumiwa huyo namba mbili, pia
wanamshukuru kwa ushirikianao uliowezesha kupatikana kwa askari huyo na
hatua kuchukuliwa dhidi yake.
"Badala
ya raia kulalamika na kusema Jeshi la Polisi halifanyi kazi ni vyema
mkatoa taarifa kama alivyotoa huyu aliyerekodi video, aliyewezesha
kumnasa aliyekuwa askari wetu na tukambaini kweli na kosa la kuomba
rushwa ya Sh. 5,000 wakati serikali inapambana na matukio kama hayo,"
alisema.
Post a Comment
Good work congratulation