Jeshi
la Magereza Tanzania limewasimamisha kazi askari wake kumi na moja
waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya mwanakijiji, Aloyce
Makalla (41) wiki iliyopita.
Taarifa
kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema askari hao walisimamishwa kazi na
Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa juzi.
Mkuu
wa Magereza Mkoa wa Tanga, John Masunga alithibitisha kusimamishwa kwa
askari hao lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi
akisisitiza kuwa msemaji wa jeshi hilo ni Kamishna Jenerali pekee.
Askari
waliosimamishwa ambao walishafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya
Korogwe mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kassim Mkwawa
ni Jonas Makere, Shadrack Lugendo, Lazaro Stephen, Mussa Zuberi,
Ramadhan Yusuf, Robert Alfred, Fhidirish Osmas, Alfonce Revocatus,
Mbesha Naftari, Hamis Msola na Michael Elias.
Taarifa
hiyo inaeleza kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi askari hao imechukuliwa
ikiwa ni kupisha vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na
kwamba hatima yao itategemea uamuzi wa mahakama hiyo.
Askari
hao wa Wilaya ya Korogwe walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa
na shtaka la kumuua, Makalla, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kerenge
wilayani humo.
Ilidaiwa
mahakamani hapo na mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Saraji Iboru
kuwa Januari 22 saa 9.30 katika kitongoji cha Mapangoni Kijiji cha
Kerenge, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanakijiji huyo.
Iboru
ambaye alikuwa akisaidiana na mwendesha mashtaka kiongozi, Shosa Naiman
alidai kwamba siku ya tukio, washtakiwa hao walikwenda nyumbani kwa
Makalla wakimtuhumu kwamba Januari 15 alimjeruhi askari mwenzao aitwaye
Sajenti Stephen.
Washtakiwa
hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na
uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji. Hakimu Mkwawa aliahirisha
kesi hiyo hadi Februari 15 itakapotajwa tena.
Post a Comment